Marekani imetaja sababu nne ambazo zimemfanya Rais Barrack Obama kuijumuisha
Tanzania katika ziara yake ya bara la Afrika.
Rais Obama amepanga kulitembelea bara la Afrika kuanzia Juni 26 hadi Julai 3,
mwaka huu na atazitembelea pia Senegal na Afrika Kusini.
Kiongozi huyo wa Marekani ambaye baba yake mzazi ni mzaliwa wa Kenya,
anatarajiwa kuwasili nchini Julai Mosi kwa ziara ya siku tatu. Atakuwa Rais wa
tatu wa Marekani kuitembelea Tanzania baada ya Bill Clinton mwaka 2000 na George
Bush mwaka 2008.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Balozi wa Marekani,
Alfonso Lenhardt alisema sababu ya kwanza ya Obama kuja Tanzania ni kutokana na
kuwa mfano wa utawala bora, demokrasia na ushirikishaji wa watu wake wakati wa
kufanya uamuzi unaogusa maisha yao ya kila siku.
Alisema kuwa Tanzania ni nchi ya mfano linapokuja suala la uongozi bora na
ndiyo maana imekuwa na amani na utulivu kwa muda mrefu ikilinganishwa na nchi
nyingi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
“Nchi nyingi za Afrika zinazoizunguka Tanzania zimekuwa na matatizo ya vita
vya wenyewe na hata ukosefu wa utawala bora,” alisema Balozi Lenhardt ingawa
alidokeza kuwa katika siku za karibuni imekuwa ikikabiliwa na changamoto
mbalimbali kutokana na matukio ya uvunjifu wa amani.
Balozi Lenhardt alisema sababu nyingine inayomfanya Rais Obama kuja Tanzania
ni kutokana na jitihada za Serikali ya Marekani kutengeneza mazingira mazuri ya
uwekezaji na kasi ya ukuaji wa uchumi.
“Rais Obama anakuja kuunga mkono juhudi za Watanzania katika kutengeneza
mazuri ya uwekezaji lakini bila kusahau kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa
Tanzania imeivutia Serikali ya Marekani,” alisema.
Balozi Lenhardt alitaja sababu nyingine inayomleta Rais Obama kuwa ni
kuisaidia Tanzania kuendeleza fursa mbalimbali za kujiletea maendeleo.
Alisema uendelezaji huo wa fursa una lengo la kuisaidia Serikali ya Tanzania
kukabiliana na tatizo la umaskini.
Alisema Marekani ni moja ya nchi zinazoongoza kwa kutoa fedha nyingi za
misaada na akisema kwa mfano, mwaka 2012 pekee ilitoa Dola 750
milioni.
Aidha, alisema nchi yake imekuwa ikitoa misaada mingi kupitia Shirika la
Millenium Challenge (MCC), ambayo imejikita zaidi katika kusaidia sekta za
umeme, maji na miundombinu.