Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amesema ni bora chama hicho kuwa na wanachama wachache walio wazuri kuliko kuwa nao wengi walio hovyo.
Kiongozi huyo wa CCM, alitoa kauli hiyo wakati akifungua mkutano wa viongozi wa matawi na mashina wa chama hicho, uliofanyika kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea juzi.
Akitoa hotuba yake mbele ya mamia waliohudhuria mkutano huo, Kinana alisema si kwamba CCM ilikuwa imeshindwa katika kata sita mjini Songea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, bali ni wana-CCM wenyewe ndio waliopoteza.
“Sio kwamba CCM ilikuwa imeshindwa kushika kata hizo bali ni baadhi ya wana-CCM ambao ni wabinafsi wenye kufikiri kuwa wengine hawawezi kuongoza isipokuwa wao ndio waliokabidhi kata hizo kwa wapinzani” alisema na kuongeza:
“Safari hii katika Uchaguzi Mkuu ujao tutakuwa wakali, bora tuwe na wana-CCM wachache walio wazuri kuliko kuwa na wengi lakini wa hovyo. Tutajiandaa kwa chaguzi zijazo kwa kupeana madarasa.”
Alisema ni marufuku kwa watendaji wa chama hicho kuwa mawakala kwa watu wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho.
Kinana aliahidi kufanya ziara rasmi katika mkoa wa Ruvuma mwezi ujao baada ya mwezi Mtukufu wa Ramadhan, aliuambia umati uliohudhuria kwamba, ili kusimamjia utekelezaji wa ahadi ambazo chama hicho kiliwahaidi Watanzania ili mwaka 2015 kiwe na la kuwaambia wananchi.
Kinana akiwa mkoani humo kwa ziara ya siku moja alishiriki shughuli maalumu ya kuwakabidhi nishani ya mwenge wa uhuru wapiganaji uhuru wa Tanganyika kwa niaba ya Rais kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment