Breaking News, Home News, international News, Comprehensive, up-to-date News coverage, aggregated from sources all over the world...

Tuesday, 11 June 2013

Marekani yataja sababu nne za Obama kuja Tanzania



Marekani imetaja sababu nne ambazo zimemfanya Rais Barrack Obama kuijumuisha Tanzania katika ziara yake ya bara la Afrika.
Rais Obama amepanga kulitembelea bara la Afrika kuanzia Juni 26 hadi Julai 3, mwaka huu na atazitembelea pia Senegal na Afrika Kusini.

Kiongozi huyo wa Marekani ambaye baba yake mzazi ni mzaliwa wa Kenya, anatarajiwa kuwasili nchini Julai Mosi kwa ziara ya siku tatu. Atakuwa Rais wa tatu wa Marekani kuitembelea Tanzania baada ya Bill Clinton mwaka 2000 na George Bush mwaka 2008.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Balozi wa Marekani, Alfonso Lenhardt alisema sababu ya kwanza ya Obama kuja Tanzania ni kutokana na kuwa mfano wa utawala bora, demokrasia na ushirikishaji wa watu wake wakati wa kufanya uamuzi unaogusa maisha yao ya kila siku.

Alisema kuwa Tanzania ni nchi ya mfano linapokuja suala la uongozi bora na ndiyo maana imekuwa na amani na utulivu kwa muda mrefu ikilinganishwa na nchi nyingi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Nchi nyingi za Afrika zinazoizunguka Tanzania zimekuwa na matatizo ya vita vya wenyewe na hata ukosefu wa utawala bora,” alisema Balozi Lenhardt ingawa alidokeza kuwa katika siku za karibuni imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali kutokana na matukio ya uvunjifu wa amani.

Balozi Lenhardt alisema sababu nyingine inayomfanya Rais Obama kuja Tanzania ni kutokana na jitihada za Serikali ya Marekani kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji na kasi ya ukuaji wa uchumi.

“Rais Obama anakuja kuunga mkono juhudi za Watanzania katika kutengeneza mazuri ya uwekezaji lakini bila kusahau kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania imeivutia Serikali ya Marekani,” alisema.

Balozi Lenhardt alitaja sababu nyingine inayomleta Rais Obama kuwa ni kuisaidia Tanzania kuendeleza fursa mbalimbali za kujiletea maendeleo.

Alisema uendelezaji huo wa fursa una lengo la kuisaidia Serikali ya Tanzania kukabiliana na tatizo la umaskini.

Alisema Marekani ni moja ya nchi zinazoongoza kwa kutoa fedha nyingi za misaada na akisema kwa mfano, mwaka 2012 pekee ilitoa Dola 750 milioni.

Aidha, alisema nchi yake imekuwa ikitoa misaada mingi kupitia Shirika la Millenium Challenge (MCC), ambayo imejikita zaidi katika kusaidia sekta za umeme, maji na miundombinu.

No comments:

Post a Comment